Recent Posts

Breaking News

BARUA YA WAZI KWA SPIKA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE. JOB NDUGAI.


Mhe. Spika,

Siyo kawaida sana kukuandikia barua kama hii lakini imenibidi kufanya hivyo. 

Lengo mahsusi ni kukuonesha masikitiko yangu na kwa kweli yanaweza kuwa masikitiko ya watanzania juu ya uamuzi wako ulioutangaza leo wa kufuta utaratibu wa bunge kuajiri wataalamu wanaoisaidia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutafiti na kuandika hotuba zake mbalimbali.

Natambua umetangaza kuwa kufutwa kwa utaratibu huo kunaihusu pia CCM kama ilivyo kwa upinzani.

Mhe. Spika,

Hakuna Mtanzania anayefurahia hayo yanayoendelea bungeni. Watanzania wengi walichukizwa sana na uamuzi wako wa kuwaondoa wabunge halali wa CUF na kuwaweka wabunge wa LIPUMBA huku ukitambua Lipumba ana mgogoro mkubwa na The Civic United Front (CUF) na tena chama kikiwa kimemfungulia yeye na Msajili wa Vyama vya Siasa kesi kadhaa.

Busara tu za kawaida zingelitosha kukataa shinikizo lolote lile (kama lilikuwepo) kutoka kwa mamlaka yoyote na kusubiri kesi mbalimbali zilizoko mahakamani zifike mwisho.

Busara zilizokosekana wakati mnashughulikia suala la CUF zingelipaswa basi kurejeshwa wakati huu wa jambo linalohusu Kambi Rasmi ya Upinzani. 

Busara hizo watanzania labda wangelipenda zipelekee wewe na wenzako kukaa kitako na kukubaliana namna bora ya kushughulikia masuala haya kuliko kuyaharibu moja kwa moja.

Mhe. Spika,

Kwa nini leo hii unaona kuwa ni sahihi kuwanyang'anya CCM na UPINZANI vijana wataalamu wa kuwasaidia kazi za utafiti na uandishi wa hotuba?

Kwa sababu, kimkakati, uamuzi huo hauiathiri CCM hata kidogo, na kwa kweli ni uamuzi ambao umekokotolewa kuua mawazo mbadala na kambi nzima ya upinzani moja moja ndani ya bunge.

Kwa mfumo wetu wa kibunge (Mfumo wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola), bunge lina kambi mbili tu; Kambi ya SERIKALI na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Ndiyo maana, hoja zikitolewa bungeni upande wa serikali unawakilishwa na Waziri Mkuu na Mawaziri, upande wa Pili ni Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tu. Hakuna upande wa tatu wala wa nne.

Hii ina maana, Waziri Mkuu na Mawaziri ambao ni wawakilishi wa chama kinachoongoza serikali wakishajibu jambo lolote moja kwa moja chama kinachoongoza dola kinakuwa kimejibu.

Kwa hiyo mabunge ya Jumuiya Madola yanakuwa na upande wa SERIKALI na wa UPINZANI, na wabunge wa chama dola wao ni sehemu ya serikali kabisa, na misimamo kwenye mambo makubwa huwa ni misimamo ya kiserikali.

Ndiyo maana kwa mfumo wetu wa kibunge, Waziri fulani akisoma hotuba ya bajeti yake (kwa niaba ya serikali) hotuba inayofuata inatoka kwa Waziri Kivuli (Kambi ya Upinzani). Wabunge wa CCM hawana hotuba rasmi mbadala ya ile ya Waziri na ndiyo maana leo umeeleza kuwa kwa mara ya tatu serikali inasoma hotuba zake, upinzani hausomi kwa hicho ulichokiita "kisingizio cha kuondolewa wasaidizi".

Mhe. Spika,

STATUS QUO ya mambo ya kibunge kwa sasa ni SERIKALI (Waziri Mkuu na Mawaziri) kufanyiwa tafiti na kufanyiwa maandishi na wataalamu walioajiriwa na serikali. Huku STATUS QUO ya Kambi ya Upinzani bungeni ikiwa ni kutofanyiwa utafiti na kutoandikiwa hotuba na wataalamu ambao kiutamaduni huajiriwa na bunge.

Ndiyo kusema kwamba, Wajibu na Majukumu ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni sawasawa na Wajibu na Majukumu ya Serikali ndani ya bunge kwa ulinganifu ule ule ndani ya bunge. 

Wajibu huo na Majukumu hayo ya Kambi ya Upinzani Bungeni haviwezi kufananishwa hata kidogo na Wajibu na Majukumu ya Kambi ya CCM (kama kambi) ndani ya bunge.

Ni kwa sababu hiyo tunaona Serikali ikitoa matamko maalum bungeni au ikisoma hotuba maalum kama za bajeti n.k. palepale Kambi Rasmi ya Upinzani nayo inasoma hotuba mbadala.

Hii ina maana, uhitaji wa vijana wa Utafiti na Maandiko kwa ajili ya kambi rasmi ya upinzani ni jambo LA LAZIMA kama ilivyo LAZIMA kwa wawakilishi wa serikali (Waziri Mkuu na mawaziri) kuwatumia wataalamu na wasaidizi ili kuandaa hotuba zao na majibu ya kila walisemalo bungeni.

Kama ndivyo basi, Serikali (Waziri Mkuu na mawaziri) ikiondolewa wataalamu wa kuisaidia kazi za kibunge (za kufanya utafiti, kuchapisha hotuba na majibu mbalimbali) hatutakuwa na hotuba za bajeti wala jambo lingine lolote. 
Mhe. Spika,

Bila wataaalamu kukaa chini na kuandaa hotuba za bajeti, hakuna waziri anayeweza kujiandalia hotuba hiyo, hayupo, maana mambo yanayowasilishwa kupitia hotuba hizo ni mambo ya kitaalamu mno na yanapaswa kutafitiwa na kujiridhisha sana. (This is a universal practice).

Sasa ikiwa hotuba za bajeti na zingine zote za serikali + matamko yote ya serikali huandaliwa na wataalamu, kwa nini serikali mbadala (Kambi Rasmi ya Upinzani) inanyang'anywa wataalamu wake na kisha mawaziri vivuli wanaelezwa "waandike hotuba zao mbadala wao wenyewe?" 

Je, mawaziri wanaweza kuandika hotuba zao za bungeni wao wenyewe? Kama mawaziri tunakubaliana hawawezi kwa nini mawaziri vivuli wanalazimishwa waweze?

Mhe. Spika,

Jambo lingine linaloshangaza ni hoja ya kulinganisha kambi rasmi ya upinzani DHIDI YA vyama visivyounda kambi hiyo. Bado jambo hili linajibiwa na hoja ile ile ya mfumo wa mabunge ya jumuiya ya madola ambako pande mbili za bunge ni (Waziri Mkuu, Mawaziri na Wabunge wa Chama kinachoongoza) DHIDI ya (Kambi Rasmi ya Upinzani).

Kwa wanaofuatilia bunge letu la Tanzania na historia yake wanajua kabisa ya kwamba chama kimoja kimoja hakikwazi mamlaka na hadhi ya kambi rasmi ya upinzani bungeni. Hata kama kambi hiyo ingelikuwa inaundwa na chama kimoja tu kwa kutimiza vigezo vya kikanuni, uongozi wa bunge unabanwa kufanya kazi na kambi hiyo kama serikali mbadala.

Kwa hiyo hatuwezi kuinyima huduma za lazima kambi rasmi ya upinzani eti kwa hoja kuwa yuko mbunge au baadhi ya wabunge hawamo kwenye kambi rasmi na kuwa tuna ushahidi kuwa wabunge hao wanao uwezo wa kuandika hotuba zao wenyewe.

Kuna tofauti ya wazi sana kati ya hotuba binafsi ya mbunge na hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Kambi Rasmi ya Upinzani ni serikali mbadala na hotuba za kambi hiyo ni hotuba mbadala za nchi. 

Hotuba ya mbunge mmoja mmoja (hata kama hayumo kwenye kambi rasmi) ni hotuba zisizo mbadala wa hotuba za serikali. Mbunge mmoja siyo serikali kivuli, Kambi Rasmi ya upinzani ndiyo serikali kivuli. 

Kuinyima kambi hii haki zake za msingi ni kuua mfumo wa kidemokrasia katika nchi, ni kudharau maoni mbadala ya wananchi na ni kulifanya bunge likose hadhi yake, hadhi ya mabunge ya Jumuiya ya Madola.

Mhe. Spika,

Uamuzi ulioutangaza leo, wa kufuta ajira za vijana wasaidizi wa kambi ya upinzani na wanaosaidia wabunge wa CCM, ni uamuzi unaoumiza upande mmoja tu, upande wa Kambi Rasmi Bungeni.

Kama nilivyofafanua, CCM hata ukiiondolea wataalamu hao hauiathiri hata kidogo, yenyewe ndiyo yenye serikali na wataalamu waliojazana kwa mamia wakitafiti na kuandika hotuba za mawaziri na Waziri Mkuu tayari wameshafanya kazi ya CCM kama chama. 

Huu ni uamuzi ambao iko haja ukautizama upya, ni uamuzi ambao unatia DOA kubwa sana katika utumishi wako na iko siku utakuja kukiri kuwa ulikuwa uamuzi wa AJABU sana ambao hayupo mtangulizi wako ambaye angelithubutu kuufanya.

Mhe. Spika, 

Ninajua ya kwamba unafanya kazi kwenye mibinyo mikubwa sana, najua kwamba unajua kwamba serikali ya awamu ya tano inafanya kila iwezalo kulifanya bunge liwe idara kamili ya serikali ili serikali ya sasa isihojiwe kabisa.

Ninajua unajua ya kwamba ili kuwa na bunge dhaifu ni pamoja na kuua kabisa nguvu, hadhi na umahiri wa kambi rasmi ya upinzani bungeni. 

Ninajua unajua ya kwamba kuipora kambi rasmi wataalamu wake ni kuidhoofisha na kuimaliza. 

Ninajua unajua ya kwamba kitendo cha leo kitasaidia sana kukamilisha mkakati wa serikali wa kutengeneza bunge lisilo na meno maana kiuhalisia sote ni mashahidi ya kwamba bunge letu kihistoria limekuwa likijenga uwezo wake na heshima yake kupitia hoja zinazoibuliwa na kambi rasmi ya upinzani, na hoja hizo huwa haziji hivi hivi, hutafitiwa na kuandikwa na wataalamu wa kambi hiyo ambao sasa wamefutwa.

Sijui kwa nini hujui na mimi sijui kwamba ni kwa nini sote hatujui kuwa uamuzi huu wa leo ni hatua muhimu za serikali kulimaliza kabisa bunge lako. Sijui ni kwa nini sote hatujui ya kwamba uamuzi huu unapaswa kupitiwa upya "to be reversed".

Mhe. Spika, 

Mimi ni kijana tu, na ni kiongozi mwandamizi wa chama cha upinzani ambacho hakina maslahi yoyote katika taifa hili zaidi ya kutaka taifa listawi na kunawiri. 

Katika umri wangu huu mdogo sana kulinganisha na wako natambua kuwa heshima ya kiongozi yeyote hupimwa kwa namna alivyosimamia nyumba yake. Bunge ni nyumba yako, watanzania wamekukabidhi -  kimantiki na kwa haki Bunge hujakabidhiwa na CCM, Rais Magufuli wala Serikali.

Bunge unaloliongoza ni bunge la watanzania. Ni sauti ya wanyonge. Spika wa Bunge ni mtu mkubwa kabisa, ana hadhi nzito kama ilivyo kwa Rais na Jaji Mkuu. 

Serikali yoyote ikiyumba, Bunge ndiyo kimbilio la wananchi. Serikali yetu kwa awamu hii imeshayumba kweli kweli, ndiyo maana kwa mara ya kwanza unawaona mawaziri wakihaha mitaani kumjibu na kumshambulia CAG bila kujali mipaka ya kazi yake. Bunge lako ndiyo kimbilio, ndiyo kanyo la mawaziri na ndiyo kipimo cha mahitaji ya sasa ya wananchi.

Kaka yangu Spika, hayo hayawezi kufanyika ikiwa wewe mwenyewe unasimama hadharani na kudhibiti au kupunguza ufanisi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni. Kazi ya kambi hii ni kukusaidia wewe kufikia malengo ya bunge la uongozi wako. Kazi ya kambi hii ni kukusaidia kujenga taswira ya bunge lako na kutetea hadhi yake kwa kuiwajibisha, kuisimamia na kuishauri serikali.

Uamuzi wako wa leo unakiuka yote, ni uamuzi mbaya, nakuomba sana, kutana na wenzako muupitie upya ulinde hadhi na heshima yako na hasa hadhi na heshima ya bunge letu ambalo ni bunge la watanzania wote. 

Mhe. Spika, nimeishiwa maneno, historia itakukumbuka vile utakavyo, kubali na omba sana historia ikuandike kwa uimara, nia njema, dhamiri safi, haki, heshima yako na ya bunge na mfano bora kabisa. Pitia uamuzi wako upya.

Wasalaam,

Julius Mtatiro,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi,
The Civic United Front (CUF),
17 Aprili 2018.

Hakuna maoni