Recent Posts

Breaking News

CUF YATOA MSIMAMO JUU YA SIKU YA HABARI DUNIANI



The Civic United Front-CUF Kinaungana na waandishi wote wa habari nchini katika kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani. CUF – Chama cha Wananchi kinatambua kwa dhati mchango muhimu na mkubwa wa waandishi wa habari katika kustawisha na kuimarisha demokrasia nchini.

Katika kuadhimisha siku hii adhimu, CUF - Chama cha Wananchi kinaendelea kuwaomba waandishi wote wa habari wa ndani na nje ya nchi kufanya kazi na kutekeleza  wajibu wao kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya habari bila ya khofu, woga na wasiwasi wa aina yoyote unaopandikizwa kwao kwa lengo la kunyamazisha sauti zao na vyombo wanavyo viwakilisha.

Aidha CUF-Chama cha Wananchi, kinatambua wazi kwamba, Tasnia nzima ya habari pamoja na waandishi wa habari Tanzania, wameendelea kufanya kazi katika mazingira magumu, yasio huru na yalio jaa vitisho na vikwazo dhidi ya kazi zao.
Kwamba, maendeleo ya tasnia ya habari yameendelea kudidimia, kutokana  na ongezeko kubwa la vitisho dhidi ya waandishi wa habari, kama kupotea, kutekwa na kupigwa hadharani kwa baadhi ya waandishi wa habari pamoja na mabadiliko ya kikanuni yanayo minya uhuru wa kutanuka kwa uhuru na upatikanaji wa habari.


CUF-Chama cha Wananchi kinatoa rai kwa wadau wa habari na Tasnia nzima kwa ujumla kuendelea kupigania uhuru wa habari kwa nguvu zote, kwasababu anguko la Tasnia ya habari ni anguko la Demokrasia na Taifa kwa ujumla.

CUF-Chama cha Wananchi kiko bega kwa bega katika kuhakikisha uhuru wa habari Tanzania unaendelea kulindwa na kuheshimiwa pamoja na kuendelea kufanya kazi kwa karibu sana na waandishi wa habari kwa maslai ya Taifa.
                              Imetolewa  leo, Tarehe 03.05.2018 Na.


MH. SALIM BIMANI
MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO YA UMMA

Hakuna maoni