Recent Posts

Breaking News

VIONGOZI WA DINI KUINGIA WOGA HATA KUSEMA UONGO.


Dini hazijaanza jana, wala siasa hazijaanza jana. Kwa Wakristo Wakatoliki, kwa woga, watu wanafuja vipaimara vyao na sakramenti ya Daraja inayowafanya wawe makuhani, manabii na wafalme hapa ulimwenguni. Hao wanapatwa na woga kiasi hiki wanasema uongo wa kwamba dini haipaswi kuhusiana na siasa.


Ni uongo kabisa kwani hata Pasaka yenyewe, tunayoisherehekea kila mwaka, ni matunda ya mwingiliano wa dini na siasa. Wayahudi wanaokolewa kutoka katika mikono ya Farao (mwanasiasa). Musa alikuwa mtu wa dini lakini alipambana na Farao, mwanasiasa. Kumbe, kudai dini isihusiane na dini siyo tu woga unaowashika viongozi wa dini isipokuwa ni pia ishara ya kutoyajua Maandiko. Tangu mwanzo wa Biblia hata mwisho wake, watu wa dini walihusiana na wanasiasa. Abrahamu alihusiana na Melkizedeki, mfalme. Tena alihusiana na Farao kule Misri hata akalazimika kusema uongo wa kwamba Sara si mkewe akiogopa kuuawa. Yusufu alihusiana kisiasa na Farao sawia na Putifa na mkewe.

Musa ndiyo tusiseme alihusiana na Farao. Mapigo kumi dhidi ya Wamisri shauri lenyewe lilikuwa siasa, utumwa. Na tunajua pigo la kumi na mbili, kuuawa kwa wazaliwa wa kwanza wa wanyama na wanadamu wa Wamisri ndilo lililo asili ya sikukuu ya Pasaka. Tupo pamoja?
Naomba niendelee na mifano. Samweli alihusiana na wanasiasa Sauli na Daudi. Elisha alihusiana na akina Ahabu na Jezebeli. Isaya alihusiana na akina Sairusi. Yeremia alihusiana na siasa za wafalme wengi hata akatupwa katika shimo la simba. Danieli na wenzake walihusiana na akina Nebukadreza na Belshaza. Manabii wote walihusiana na wafalme ama wakiwaunga mkono na kuwashauri au kuwaonya na kuwasahihisha. Yohane Mbatizaji alimkanya mwanasiasa Herodi Antipasi akalipia kwa shingo lake. Yesu mwenyewe alihusiana na wanasiasa kama akina Herode na Pilato. Mbona tunakumbuka kwamba Yesu alihukumiwa na Pilato,
Hatimaye, mitume nao walihusiana na wanasiasa, wengine wakali sana wakawatoa roho zao. Hata kitabu cha mwisho cha Biblia (ndiyo Ufunuo) ni mahusiano kati ya Dola ya Rumi na Wakristo. Makaisari walikuwa wanasiasa. Kaisari Konstantino aliyelisaidia Kanisa kupata nafuu ya madhulumu alikuwa mwanasiasa. Je, hatumsifu kwa kuwa mtu mwema?
Baada ya mitume, watakatifu mbalimbali walihusiana pia na wanasiasa kwa kuwaunga mkono au kuwakanya. Akina Thomas More na John Fisher walipotezaje maisha yao? Maximilian Kolbe alikufa katika muktadha gani? Kwa nini Baba watakatifu walioishi wakati wa biashara ya utumwa na hata wakati wa mauaji ya kimbari yaliyoendeshwa na Adolf Hilter dhidi ya Wayahudi wanalaumiwa kwa kutokuwa na misimamo ya kuwatetea wanyonge?
Si hivyo tu, historia ya Kanisa imejaa hati zinazohusika na mambo ya siasa. Rerum Novarum ina muktadha upi? Gadium et Spes ina muktadha gani, kwa nini tuseme Kanisa Ulimwenguni? Ulimwengu wa wapi wanaoishi wanadini peke yao pasipo dola, nchi na mataifa? Sasa inakuwaje ajabu au haramu kwetu sisi tunaoishi katika karne hii kujihusisha kwa namna yake na siasa?
Tusijipinge wenyewe. Kwa nini kila tunaposali sala za waumini tunaiombea serikali na viongozi wao? Tunawaombeaje ikiwa mambo yao hayatuhusu? Lakini ukweli ni huu. Tunaishi katika ulimwengu mmoja na wanasiasa. Ni katika ulimwengu huo huo tunamoaswa kufanya utume. Yesu Kristo hajawapa Wakristo ulimwengu wao peke yao (Yn 16:33).
Kama ndivyo, tutawezaje kuzungumzia mambo ya haki, amani na upatanisho pasipo kuwagusa wanasiasa na watawala ambao ndio wenye vyombo vinavyohusika na hayo? Anawezaje mwanadini kuzungumzia haki bila kuigusa nchi na watawala wake? Anawezaje mwanadini kuzungumzia haki na amani pasipo kuwagusa polisi na mahakimu?

Nadhani kama Wakristo wasingelikuwa raia wa nchi za ulimwengu huu na wanasiasa wasingelikuwa waamini wa dini za ulimwengu huu, dini na siasa vingeliweza kutenganishwa vizuri kabisa. Lakini kama waamini tusingelikuwa raia tusingelilipa kodi na wala tusingelishiriki chaguzi zozote na wanasiasa nao wasingelikuwa waamini tusingeliwatazamia waje kusali wala kushika amri yoyote ya Mungu.

Kumbe basi, woga wetu usitufanye tuseme uongo wa kutaka dini na siasa visigusane, tunamuumiza sana Yesu aliyekuwa jasiri namba moja.



Ukweli ni kwamba wanadini siasa inatuhusu na wanasiasa dini inawahusu. Nani aliyesema mwanadini hawezi kuwa mwanasiasa na mwanasiasa hawezi kuwa mwanadini? Tusipotoshe mambo kwa woga wetu. Kumbe, kinachohitajika ni busara na kujali uwiano wa kusifiana, kuhimizana, kujadiliana na kuonyana ili wote tusiukose uzima wa milele. La sivyo, waamini na viongozi wao wasiseme wanashiriki ofisi za unabii na ufalme za Yesu Kristo!

Aidha, kukutana dini na siasa si ajabu. Kama tumetumwa ulimwenguni tukawafanye watu wote wanafunzi wa Yesu tusistaajabu kukutana na wafanyabiashara, wanasiasa, wema na wabaya. Acha nikumbuke wimbo wa zamani. Ni hivi kila mwamini, kwa sababu ya utume wake wa kimisionari ambao kwao anatakiwa kukutana na watu wote, anapaswa kujiimbisha wimbo wa zamani wa “Wote ni abiria wangu”, maana yake wanasiasa na siasa zao wamo kati ya abiria wake.*
Ndimi mzee wenu Pd. Titus Amigu.

Hakuna maoni