Muungano wa zanzibar na Tanganyika bado ni kaa la moto
TAMKO RASMI April 11, 2018. Jumuiya Ya Wazanzibari Waishio Nchini Marekani (ZADIA), inapenda kuungana na Wazanzibari wote, ndani na nje ya Zanzibar, katika kuunga mkono msimamao madhubuti wa kizalendo uliodhihirishwa na Wabunge kutoka Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Itakumbukwa kuwa mnamo siku ya Jumatatu tarehe 09 April, 2018, Wabunge kutoka Zanzibar, bila kujali itikadi zao za kisiasa, walitoka nje ya Bunge wakati wa kikao cha Bajeti ya Waziri Mkuu wakilalamikia kudhalilishwa kwa hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano na ndani ya Bunge hilo.
ZADIA inaamini kuwa Tanzania ni Muungano wa nchi mbili zenye hadhi sawa, (Tanganyika na Zanzibar) zilizoungana na kuunda kilichojulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na baadae Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba Serikali ya Tanzania haina mamlaka juu ya Serikali ya Zanzibar yenye Taasisi zake kamili na imara. Kwa hivyo inaunga mkono kauli ya Wabunge hao Wazalendo waliyoitoa wakiongozwa na Mheshimiwa Ally Saleh (Mbunge – CUF Malindi, Zanzibar) kupinga vitendo na kauli za kuidhalilisha Zanzibar ndani ya Bunge na katika Serikali ya Tanzania. Aidha, ZADIA inapenda kutoa pongezi rasmi kwa Mheshimiwa Sada Mkuya (Mbunge – CCM Welezo, Zanzibar) kwa ujasiri wake wa kusimama kidete na kutetea hadhi na maslahi ya Zanzibar ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunapenda kumthibitishia kuwa Wazanzibari wote, bila kujali tofauti zao za kisiasa, kijinsia na nyenginezo wako pamoja naye katika mapambano ya kupigania haki na hadhi ya Zanzibar tuipendayo ndani ya Muungano wa Tanzania na duniani kote.
Hakuna maoni